2022 Mei 23 Jumatatu: Juma la 6 la Pasaka

SOMO 1: Mdo. 16:11-15
Tuling’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, “Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae.” Akatushurutisha.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 149:16, 9

Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K)Bwana awaridhia watu wake.Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wote. (K)

INJILI: Yn. 15:26-16:4
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami. Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.”

TAFAKARI
BURIANI, TAHADHARI NA AHADI ZA KRISTO: Kristo anatoa buriani, ambayo ni tahadhari na ahadi zake kwa mitume. Anatanguliza kuondoka kwake, anawaahidi ujio wa Msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu atakayemshuhudia pamoja nao na kuwaimarisha, na anatoa tahadhari kwamba mitume watakumbwa na pingamizi. Buriani ya Yesu kwa mitume wake na taarifa ya dhiki zijazo linawatia hofu. Lakini ahadi ya ujio wa Msaidizi zinawapa matumaini. Somo la kwanza linaonyesha sehemu ya kazi iliyofanywa na mitume baada ya matukio haya yaliyotabiriwa na Kristo kutimia. Kwa kuongozwa na Roho mtakatifu wanaeneza Habari Njema kwa ushujaa. Pia wanakutana na faraja ya watu wema wanaowahudumia na kuwakaribisha kwao.
Kwa kuamini ahadi hizi za Kristo Mfufuka, nasi pia Mungu anatufariji tunapojikuta katika unyonge na upweke katika kutekeleza utume wetu. Kristo yupo karibu na wanaomtumainia.

SALA: Ee Bwana, Roho Mtakatifu na awe kwetu faraja na nguvu, tusiogope kuishuhudia injili.

Post a Comment

0 Comments