Ad Code

Masomo ya misa jumamosi



SOMO 1: Gal. 3:22-29

Andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 105: 2-7

Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. (K)
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)
Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

INJILI: Lk. 11:27-28

Ikawa, Yesu alipokuwa akisema, “Mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, ‘Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya.’” Lakini yeye alisema, “Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.”

TAFAKARI
UMUHIMU WA IMANI THABITI: 
Katika somo la kwanza Paulo anawakumbusha na kuwasisitiza Wagalatia wadumu katika imani yao kwa Mungu kwani ni katika imani hiyo walibatizwa na kumvaa Kristo. Ni katika imani hiyo umoja wa kweli umeonekana kwani wote waliobatizwa wamekuwa watoto wa Mungu. Katika Injili, imani imemfanya mawanamke aliyemsikiliza Yesu kwa makini amsifu mama aliyemzaa na kumnyonyesha. Yesu, ili kuwaondolea mawazo ya ubinafsi, anasema kuwa heri zaidi walisikialo neno la Mungu na kulishika. Sisi tuna bahati ya kulisikia Neno la Mungu katika makanisa, vyombo vya habari, mitandao, makongamano na semina. Tunaposikiliza Neno hilo tufanye mabadiliko chanya kuhusu maisha yetu ya kiroho kwa kuishi tunu zinazoambatana na mapenzi yake Mungu. Tumwombe Mungu ili sisi ambao tumeshalisikia Neno la Mungu na kulipokea tuweze kuzama katika imani, tuweze kumpendeza, kumwabudu na tupate wokovu.

SALA: Ee Yesu, tunaomba utuongezee imani. Amina.

Post a Comment

0 Comments