Ad Code

MASOMO YA MISA MEI 11, 2023; ALHAMISI: JUMA LA 5 LA PASKA

Mt. Fransisko Di Girolamo, Padre

Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mdo 15:7-21
Wakati wa mtaguso wa Yerusalemu, baada ya hoja nyingi Petro alisimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao. Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa. Baada ya mambo haya nitarejea, nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, nami nitaisimamisha; ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila Sabato katika masinagogi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 96:1-3, 10

  1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
    Mwimbieni Bwana nchi yote.
    Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake.
    (K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.
  2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
    Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
    Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
  3. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
    Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
    Atawahukumu watu kwa adili. (K)

INJILI: Yn 15:9-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.

TAFAKARI:
TUDUMU KATIKA UPENDO WA MUNGU KWA KUTIMIZA MAPENZI YAKE: Katika jumuiya zetu, tuna watu ambao wapo kifua mbele kutetea amani na usawa katika maisha ya jumuiya. Wanajitoa sana kwa hili wakitamani kuona kuwa jumuiya ina umoja, amani na upendo. Mtume Petro katika somo la kwanza, anapambana na hatimaye anafanikiwa kuleta usawa katika Kanisa la mwanzo. Anawafanya Wakristo wasio na asili ya Kiyahudi kutolazimishwa kufuata mila za Kiyahudi. Tutambue wazi kuwa Kristo anataka tudumu katika upendo wake. Kama vile Baba ampendavyo Yeye, ndivyo nasi tunapaswa kupendana. Kwa kuhimiza umoja na mshikamano kati ya Wakristo wa mwanzo wanaotoka kwenye makabila na tamaduni tofauti, Mtume Petro anakuwa mfano mwema wa mtu anayewaunganisha wote wanaomfuata Kristo kutoka mataifa na lugha tofauti. Basi tunaalikwa leo kuwaona watu wote kuwa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Hivyo hatupaswi kuwabagua bali kuwapenda katika mambo yote ili waonje upendo wa Mungu kupitia kwetu, nao waueneze kwa wengine.

SALA:Tuombe neema ili tudumu daima katika upendo wa Mungu ili dunia ibaki na amani. Amina.

Post a Comment

0 Comments