Ad Code

MASOMO YA MISA MEI 15, 2023; JUMATATU: JUMA LA 6 LA PASAKA

Mt. Isidori
Nyeupe

Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mdo 16:11-15
Tuling’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya Sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 149:16, 9

  1. Aleluya.
    Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
    Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
    Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
    Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
    (K)Bwana awaridhia watu wake.
  2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
    Kwa matari na kinubi wamwimbie.
    Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
    Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
  3. Watauwa na waushangilie utukufu,
    Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
    Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
    Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wote. (K)

INJILI: Yn 15:26-16:4
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami. Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.

TAFAKARI:
MUNGU ROHO MTAKATIFU ATUANGAZIE NEEMA YA KUUSHUHUDIA UKWELI

Daima tunapopewa wasaidizi au misaada ya kutuongoza huwa tunafurahia sana, kazi zetu daima huwa nyepesi na mzigo hupungua uzito wake. Mtume Paulo anazidi kupambana kuieneza Injili kwa watu katika mazingira yote ya kukataliwa, kusimangwa na hata kuteswa lakini hakati tamaa bali anaendelea kwa kasi kubwa ajabu akiongozwa na Roho Mtakatifu. Bwana wetu Yesu Kristo anapambanua wazi uzito na ugumu wa kazi wanayoiendea, yaani kulitangaza Neno la Mungu, anawapa wafuasi wake matumaini ili wasikate tamaa kwa kazi ya Mungu wanayoifanya, anawapa ujasiri kuwa Mungu Roho Mtakatifu atawafundisha yote ili waishuhudie ile kweli na wazidi kumjua Mungu nyakati zote na kuwaambia wengine habari za Mungu. Wapendwa katika Kristo, sisi kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara tulimpokea Roho Mtakatifu ili atuangaze katika maisha yetu ya Kikristo na kuwafanya wengine wamtambue na kumjua Mungu na mwisho, sote tufike Mbinguni. Basi tutimize wajibu huo bila woga wala kukata tamaa.

SALA: Mungu Roho Mtakatifu tunaomba utuangazie neema ili tuzidi kumshuhudia Kristo kwa watu wote. Amina.

Post a Comment

0 Comments