Nyeupe
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mdo 15:1-6
Siku zile, walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo. Basi, wakisafirishwa na Kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao mataifa; wakawafurahisha ndugu sana. Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na Kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao. Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 122:1-5
- Nalifurahi waliponiambia
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu.
(K)Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana. - Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ule ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K) - Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)
INJILI: Yn 15:1-8
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.
Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.
Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
TAFAKARI:
UMOJA HULETA AFYA MAISHANI: Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Raisi wa kwanza wa Muungano wa Tanzania, aliwahi kuieleza dhambi ya ubaguzi kuwa mbaya sana. Alielezea kuwa mtu aanzapo kuitenda, hushiindwa kuiacha hadi pale inapomwuumiza mwenyewe. Mwenyezi Mungu alipotuumba wanadamu alitaka tuwe wamoja tukiwa kwenye makabila, mila na desturi zetu, na katika yote tumjue, tumwamini, tumtumikie na mwishoni tufike kwake Mbinguni. Kila mila na desturi zilizo njema, hazina budi kutusogeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kumuishia Kristo. Kabla ya kuitwa kuwa Wakristo, tunazo desturi na mila zetu. Ila tuitwapo, tunaagizwa kuzifuata mila na desturi zake Kristo. Tutazifuata tu mila na desturi zetu pale ambapo hazipingani na Ukristo. Ndio maana, Mitume; Paulo na Barnaba, baada ya kuona watu wa mataifa wanamgeukia Mungu, wanawapokea pamoja na mila na desturi zao njema huku wakiwatetea wasilazimishwe kumpokea Kristo na mila za kiyahudi (Kutahiriwa). Tutambue wazi kuwa sisi tulio matawi, sharti tuungane na Kristo aliye Mzabibu. Tukizifuata mila na desturi zake Kristo, aliye shina, tutapata chakula cha kimwili na cha kiroho. Kwa kuheshimu mila njema, kila mmoja wetu, aunganishwe Kristo, na sote tudumu ndani yake Kristo aliye Mzabibu.
SALA: Tuombe neema kwa Mungu ili kwa kuungana na Kristo, tuzae matunda mema yatupasayo wokovu. Amina.
0 Comments