SOMO 1: Mdo. 13:44-52
Paulo na wenziwe waliingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 98:1-4
- Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu. - Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K) - Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
INJILI: Yn. 14:7-14
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.
TAFAKARI:
TUMSADIKI KRISTO KWANI NDIYE MSAADA WETU: Paulo na wenzake wanatoa ushuhuda juu ya Kristo na kufundisha mafundisho yaliyo ya Kristo mwenyewe, licha ya upinzani kutoka kwa viongozi na kundi zima la Wayahudi. Hawa wapinzani wanachichea kuwa wakisemacho akina Paulo, si kweli. Ndiyo maana Paulo anawaambia kuwa, kwa kuwa hawapo tayari kulipokea Neno, watawapelekea watu wa mataifa mengine. Nyakati tofauti nasi hujipata kwenye hali kama hiyo: hatutaki kuikubali Habari Njema ya Kristo, hata na wajumbe wenyewe. Hujipata tunavutiwa na mengineyo ya kidunia. Katika Injili, Yesu anamjibu Filipo kwa kusema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu?” Maneno haya yatuhimize kumsadiki Kristo kwani kwa njia hiyo twamsadiki Mungu Baba. Tuwe tayari kumfuata Kristo katika utume wetu wala tusikate tamaa. Tumtangaze kwa watu wote hata wale ambao jamii zetu zinawaona hawafai, ili nao walisikie Neno lake, waliamini na waliishi daima.
SALA: Ee Mungu tunakuomba utupe mwanga wa kumsadiki na kumwomba Kristo aliye kimbilio katika shida zetu, amina.
0 Comments