Ad Code

MASOMO YA MISA JUNI 16, 2023; IJUMAA: JUMA LA 10 LA MWAKA

MOYO MTAKATIFU WA YESU

Sherehe
Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Kum. 7:6-11
Musa aliwaambia makutano: Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako; Bwana Mungu wako amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi. “Bwana hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote; bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri. Basi, jueni ya kuwa Bwana Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu; naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, ili kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipia mbele ya uso wake. Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazoamuru leo, uzitende.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 103:1-4, 6-8, 10

  1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana
    Naam, vyote vilivyo ndani yangu
    Vilihimidi jina lake takatifu.
    Ee nafsi yangu, umuhimidi Bwana,
    Wala usizisahau fadhili zake zote.
    (K) Fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele.
  2. Akusamehe maovu yako yote,
    Akuponya magonjwa yako yote,
    Aukomboa uhai wako na kaburi,
    Akutia taji la fadhili na rehema. (K)
  3. Bwana ndiye afanyaye mabo ya haki,
    Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
    Alimjulisha Musa njia zake,
    Wana wa Israeli matendo yake. (K)
  4. Bwana amejaa huruma na neema,
    Haoni hasira upesi ni mwingi wa fadili.
    Hakututendea sawasawa na hatia zetu,
    Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.(K)

SOMO 2: 1 Yoh. 4:7-16
Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu: kwamba Mungu amemtuma mwanawe pekee ulimwenguni ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.

SHANGILIO: Mt.11:29
Aleluya, aleluya,
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu,
kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
Aleluya

INJILI: Mt. 11:25-30
Wakati ule Yesu alijibu, akasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.” Akasema, “Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

TAFAKARI:
Tazama Moyo uliotoka Damu kwa Ajili ya kuwapenda watu: Leo tunaadhimisha sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hapo mwaka wa 1856 Baba Mtakatifu Pius wa tisa, aliiweka sherehe hii katika Kalenda ya Kanisa. Alifanya hivi baada ya karne mbili za ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwenye sherehe hii tunaadhimisha upendo wa Mungu ulio katika nafsi ya Yesu Kristo. Tunalo wazo la upendo, kama wanadamu. Ndipo sisi hutumia semi kama vile ‘nakupenda kwa moyo wangu wote’ na hata Februari 14 tunaadhimisha siku ya wapendanao. Ila leo, upendo tunaoutafakari ni wa kina zaidi. Ni upendo wa Mungu kwa watu wake, na upendo mkubwa wa Yesu kwetu sisi. Hakuna tunaloweza kulifanya ili Mungu atupende zaidi au aupunguze upendo wake kwetu; upendo wake hauna mipaka wala kipimo. Inaaminika kuwa moyoni ndimo udumuo upendo. Kwa hiyo moyo unafananishwa na roho, upendo, nguvu, ukarimu, na kwa ujumla wake, moyo unawakilisha nafsi nzima ya mtu. Moyo Mtakatifu wa Yesu unatufundisha kwamba Mungu anatupenda zaidi ya wazazi wawapendavyo wana wao, zaidi ya rafiki yeyote yule. Tunaupenda Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwa sababu Moyo wake umetupenda sisi kwanza. Ukristo unapaswa kuutangazia ulimwengu kuwa Mungu ni upendo. Upendo huu ndio ulimfanya Yesu kuinyoosha mikono yake akafa msalabani kwa ajili yetu. Mt. Margareta Maria na Mt. Maria Faustina, wanauonyesha upendo huu mwao maishani. Upendo huu umejawa na bahari ya msamaha wa Mungu, unaowasubiri wote wanaotubu. Tafakari ya leo inayaleta pamoja mambo matatu: Moyo Mtakatifu wa Yesu, Upendo na Huruma. Moyo wa kweli kati ya wanadamu huonekana palipo na shida na mateso, kwenye mahitaji na ugonjwa. Tudumu katima kutenda wema tukiuangalia upendo mkuu wa Yesu uliomfanya atufie msalabani. Huu ndio Moyo wa Kweli, Moyo ulio Mtakatifu. Katika sherehe ya leo, tuonyeshe shukrani zetu, kwa Bwana, kwa upendo anaoendelea kutuonyesha daima. Nasi tumwahidi kuwapenda wenzetu kwani pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu.

SALA: Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunaomba, tunatafuta na tunabisha, tukiwa na hakika na matumaini, kwamba utatusikia na kutujibu ili tuwe wenye upendo wa dhati. Amina.

Post a Comment

0 Comments