Ad Code

MASOMO YA MISA, JUNI 2, 2023 IJUMAA, JUMA LA 8 LA MWAKA

SOMO 1
Ybs 44:1, 9-13

Haya na tuwasifu watu wa utauwa, Na baba zetu katika vizazi vyao. Baadhi yao hawana kumbukumbu, Wamepotea kana kwamba hawakuwako; Wamekuwa kana kwamba hawakuzaliwa, Wala watoto wao; Lakini hawa walikuwa watu wa utauwa, wala kazi zao za haki hazisahauliki. Wema wao utawadumia wazao wao, Na urithi wao una wana wa wana; Wazao wao wanashikamana na agano, Na watoto wao kwa ajili yao. Kumbukumbu lao litadumu milele, Wala haki yao haifutiki kamwe;

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI 
Zab 149:1b-2, 3-4, 5-6, 9

(K) Bwana awaridhia watu wake.

Mwimbieni Bwana wimbo mpya, 
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya, 
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.

Na walisifu jina lake kwa kucheza, 
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake, 
Huwapamba wenye upole kwa wokovu.

Watauwa na waushangilie utukufu, 
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. Aleluya.



SHANGILIO 
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya, 
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika. 
Aleluya.



INJILI 
Mk. 11:11-26

Yesu aliingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara.

Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipouiikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.

Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza na wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akasema, Je! haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini.

Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akawaambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.

Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, ntkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo. 

Post a Comment

0 Comments