Ad Code

MASOMO YA MISA, JUNI 20, 2023 JUMANNE, JUMA LA 11 LA MWAKA


SOMO 1
2 Kor. 8:1 – 9

Ndugu zetu, twaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.

Hata tukamwonya Tito kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha. Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 146:2, 5 – 9 (K) 2

(K) Ee nafsi yuangu, umsifu Bwana.

Ee nafsi yangu umsifu Bwana
Nitamsifu Bwana muda ninaoishi,
Nitamwimbia Mungu wangu ningali hai. (K)

Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake,
Aliyezifanya mbingu na nchi,
Bahari na vitu vyote vilivyomo. (K)

Huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula,
Bwana hufungua waliofungwa. (K)

Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
Bwana huwainua walioinama,
Bwana huwapenda wenye haki
Bwana huwahifadhi wageni,
Huwategemeza yatima na mjane. (K)



SHANGILIO
Ebr. 4:12

Aleluya, aleluya.
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.



INJILI
Mt. 5:43 – 48

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, pendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyk, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

0 Comments