Ad Code

MASOMO YA MISA, JANUARI 18, 2025 JUMAMOSI, JUMA LA 1 LA MWAKA


SOMO 1
Ebr. 4:12 – 16

Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na ivungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.

Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:7 – 9, 14 (K) Yn. 6:63

(K) Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako.

Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako,
Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
Umempa haja ya moyo wake,
Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake. (K)

Maana umemsogezea Baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
Alikuomba uhai, ukampa,
Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele. (K)

Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako,
Heshima na adhama waweka juu yake.
Maana umemfanya kuwa Baraka za milele,
Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako. (K)


SHANGILIO
Lk. 4:18 – 19

Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma kuwahubiri maskini habari njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.
Aleluya.


INJILI
Mk. 2:13-17

Yesu alitoka, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata.

Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi wa wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata. Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

0 Comments