MWANZO:
Zab. 31:2 – 4
Uwe kwangu mwamba wa nguvu, nyumba yenye maboma ya kuniokoa. Ndiwe genge langu na ngome yangu; kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.
SOMO 1
Yer 7:5-8
Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema; bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji. Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 1:1 – 4, 6 (K) 39:5
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, wala hakuelekea wenye kiburi.
Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shuri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)
Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SOMO 2
1Kor. 15:12, 16-20
Ikiwa Kristu anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalipo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Efe. 1:17-18
Aleluya, aleluya.
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, uyatie nuru macho ya mioyo yetu, ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.
INJILI
Lk. 6:17, 20-16
Yesu alishuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.
Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile n akurukaruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni; maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo.
Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 Comments