Ad Code

MASOMO YA MISA, FEBRUARI 6, 2025 ALHAMISI JUMA LA 4 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA WAT. PAULO MIKI NA WENZAKE (MASHAHIDI)


SOMO 1
Ebr. 12:18-19, 21-24

Ndugu zangu hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lolote linguine. Na hayo yalionekana jinsi yalivyokuwa ya kutisha, hata Musa akasema, Nimeshikwa na hofu na kutetemeka. Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 48:1-2, 8-10 (K) 9
(K) Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu, katikati ya hekalu lako.
Bwana ndiye aliye mkuu,
Na mwenye kusifiwa sana,
Katika mji wa Mungu wetu.
Katika mlima wake mtakatifu.
Kuinuka kwake ni mzuri sana,
Ni furaha ya dunia yote. (K)
Mlima Sayuni pande za kaskazini,
Mji wa mfalme mkuu.
Mungu katika majumba yake
Amejijulisha kuwa ngome. (K)
Kama tulivyosikia, ndivyo tulivyoona,
Katika mji wa Bwana wa majeshi,
Mji wa Mungu wetu,
Mungu ataufanya imara hata milele. (K)
Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu,
Katikati ya hekalu lako.
Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu,
Ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia,
Mkono wako wa kuume umejaa haki. (K)

SHANGILIO
Zab. 147:12,15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
INJILI
Mk. 6:7-13

Siku ile Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu, akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali popote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali popote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

0 Comments