JUMATANO, JUMA LA 1 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 2:14 – 18
Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.; maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105:1 – 4, 6 – 9 (K) 8
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo yake.
Mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote. (K)
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana,
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote. (K)
Enyi wana wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo wateule wake.
Yeye Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
Analikumbuka agano lake milele,
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
Na uapo wake kwa Isaka. (K)
SHANGILIO
Efe. 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
INJILI
Mk. 1:29-39
Siku ile, Yesu alipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohane. Naye mkewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.
Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.
Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea. Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 Comments