Ad Code

MASOMO YA MISA, APRILI 23, 2022

JUMAMOSI KATIKA OKTAVA YA PASKA
SOMO 1

Mdo. 4:13 – 21

Siku ile, makuhani na akida wa hekalu walipoona ujasiri wa Petro na Yohane, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu. Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tuwafanyieni watu hyawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana. Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohane wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka.


Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI

Zab. 118:1, 14 – 21 (K) 21


(K) Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

Au Aleluya


Aleluya,

Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,

Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,

Naye amekuwa wokovu wangu.

Sauti ya furaha na wokovu,

Imo hemani mwao wenye haki. (K)


Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.

Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;

Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.

Sitakufa bali nitaishi,

Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.

Bwana ameniadhibu sana,

Lakini hakuniacha nife. (K)


Nifungulieni malango ya haki,

Nitaingia na kumshukuru Bwana.

Lango hili ni la Bwana,

Wenye haki ndio watakaoliingia.

Nitakushukuru kwa maana umenijibu,

Nawe umekuwa wokovu wangu. (K)


SHANGILIO

Zab. 118:24


Aleluya, aleluya,

Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutaishangilia na kuifurahia.

Aleluya.


INJILI

Mk. 16:9 – 15


Yesu alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba. Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki.

Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba. Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki.

Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.


Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo....

Post a Comment

0 Comments