Ad Code

𝗙𝗔𝗛𝗔𝗠𝗨 𝗠𝗔𝗔𝗡𝗔 𝗬𝗔 𝗝𝗨𝗠𝗨𝗜𝗬𝗔 𝗡𝗗𝗢𝗚𝗢 𝗡𝗗𝗢𝗚𝗢 𝗡𝗔 𝗖𝗛𝗜𝗠𝗕𝗨𝗞𝗢 𝗟𝗔𝗞𝗘.

✦ Jumuiya ndogo ndogo ni kikundi kidogo cha Wakristo hasa Wakatoliki waliotoka kwenye familia mbalimbali zilizo jirani, ili kukusanyika pamoja kwa ajili ya kusali na kushirikishana Neno la Mungu nyumba kwa nyumba.

✦ Chimbuko la Jumuiya ndogo ndogo katika Biblia ilikuwepo tangu zamani, ambapo Wakristo wa mwanzoni kabisa walikutana na kumega mkate nyumba kwa nyumba, desturi ambayo ipo hadi leo.

• Matendo ya Mitume 2:42-47

"Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, walimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, huku wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha Kanisa kila siku, kwa wale waliokuwa wakiokolewa"

• Matendo ya Mitume 4:32

"Wakawa wakidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika, na katika kumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa hofu, ajabu nyingi na ishara zikafanywa na Mitume. Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia wote kama kila mtu alivyokuwa na haja"

✦ Lakini mwaka 1976 baada ya Mkutano wa AMECEA, jumuiya hizi zikazaliwa na kuanzishwa katika maeneo yote ya Afrika Mashariki, hasa zaidi katika nchi ambazo zimefungamana na shirikisho hili. Kwani mpaka kufikia mwaka 2001 tafiti zinasema, kulikuwa na jumuiya ndogo ndogo zipatazo zaidi ya 180,000 katika nchi nane za AMECEA ambazo ni:

1. Tanzania
2. Kenya
3. Uganda
4. Ethiopia
5. Sudan
6. Eritrea
7. Malawi
8. Zambia

✦ Ukweli jumuiya hizi hujengwa na familia kadhaa, zisizopungua tano wala kuzidi kumi na tano. Familia hizi hushirikiana katika mambo yote hasa ikiwemo kusali, kutafakari Neno la Mungu, kusaidiana wakati wa shida, kufarijiana wakati wa misiba, kulea watoto n.k

𝗨𝗠𝗨𝗛𝗜𝗠𝗨 𝗪𝗔 𝗝𝗨𝗠𝗨𝗜𝗬𝗔 𝗡𝗗𝗢𝗚𝗢 𝗡𝗗𝗢𝗚𝗢

1. Hutuimarisha kiroho hasa pale tunapolisoma Neno la Mungu, na kulitafakari kila mara.

2. Ni chachu ya ushirikiano na umoja ndani ya Kanisa, na jamii yote kwa ujumla.

3. Ni sehemu ya kusaidiana na kufarijiana katika changamoto mbalimbali, ikiwemo za maradhi, misiba, umaskini n.k

4. Husaidia kulea vijana na watoto katika miito na maadili mema, ili kuwa Watumishi bora wa Kanisa na taifa.

5. Ni sehemu rahisi ambayo kila Muumini anaweza kutoa maoni, ushauri au mapendekezo kuhusu Kanisa.

6. Hutumika kutatua migogoro mbalimbali kwa Wanandoa, kwa utaratibu unaofaa kabla ya kwenda kwa Paroko.

7. Ili kupata huduma ya Kanisa, mfano kubatiza watoto, kubariki ndoa n.k ni lazima uanzie katika ngazi ya jumuiya.

8. Viongozi wote wa halmashauri ya walei ngazi ya parokia, dekania, jimbo hadi taifa, lazima waanzie katika jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.

9. Inakuza imani na maadili ya Kikristo kwa familia, hasa ile ambayo Baba, Mama, Watoto na Ndugu wanaishi pamoja kama wakishiriki jumuiya kikamilifu.

10. Husaidia kumtangaza Kristo kwa wasio Wakatoliki, hasa pale jumuiya inapotoa misaada mbalimbali ya fedha, chakula, nguo n.k katika jamii inayowazunguka.

✦ Hivyo ndugu zangu niwasihi tu kuwa, jumuiya ndiyo kila kitu kwa Mkatoliki. Kwahiyo usipange hata siku moja kuacha kwenda jumuiyani, kama hauna kizuizi chochote cha umuhimu.

𝗝𝘂𝗺𝘂𝗶𝘆𝗮 𝗻𝗱𝗼𝗴𝗼 𝗻𝗱𝗼𝗴𝗼, 𝘂𝗵𝗮𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝗮𝗻𝗶𝘀𝗮.

Post a Comment

0 Comments