Paulo na Barnaba wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini. Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia. Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia. Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza. Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:8-13
- Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
- Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K) - Ili kuwajulisha watu matendo yako makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
SOMO 2: Ufu. 21:1-5a
Siku ile, mimi, Yohane, niliona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao. Wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.
SHANGILIO Yn. 13:34
Aleluya, aleluya,
Bwana asema: Amri mpya nawapa,
Mpendane, kama vile nilivyowapenda ninyi.
Aleluya.
INJILI: Yn. 13:31-33a, 34-35
Yuda alipokwisha kutoka, Yesu alisema, “Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara. Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi. Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”
TAFAKARI
UPENDO UNGEKUWA KUSEMA TU TUSINGELISHINDWA: Wazo hili linatoka kwenye Injili nalo linaungwa mkono na masomo mengine mawili yaliyosomwa hivi punde. Injili imechukuliwa katika Yohane 13, sura ambayo ni mwanzo wa sura zinazoripoti mipango na sala za Yesu saa chache kabla ya kukamatwa kwake. Yu katika muktadha wa karamu ya mwisho. Katika nyakati hizo za mwisho Yesu alijua mambo yanavyoendelea na hivyo kujua kwa uhakika kwamba si muda mrefu ujao angekamatwa, angeteswa, angesulibiwa, kufa na kuzikwa, lakini angefufuka baada ya siku tatu.
Kwa kuwa alitaka kuyatimiza mapenzi ya Baba, alituliza kichwa na kutoa maagizo mbalimbali ili kuteswa na kufa kwake kusizime mradi wa ukombozi. Akafundisha na kuweka mambo mengi sawa. Kati ya mambo hayo ilikuwa kuagiza amri ya upendo iwatambulishe wanafunzi wake. Akawapa amri hiyo kama amri mpya, wapendane. Wengine huuliza kwa nini Yesu aliite upendo amri mpya? Kuna sababu tatu kwa nini amri ya upendo iitwe mpya. Inakuwa amri mpya kwa sababu wanafunzi wake wanaishika amri hiyo katika enzi mpya (Agano Jipya), kwa mfano mpya (yeye mwenyewe) na kwa mapana mapya (ndiyo kuwapenda hata adui zao).
Ukikusanya maneno ya Yesu katika Injili ya Yohane na Injili zote, utagundua kwamba amri ya upendo ingekuwa maneno tu, tusingalishindwa kuishi kiufanisi, lakini inahusisha matendo. Kwa amri ya upendo kuna kuna kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Kuna matendo matano kumwelekea Mungu na matendo kumi na manne kumwelekea jirani. Kumwelekea Mungu ni: kumwabudu, kusali, kuweka nadhiri au ahadi na kuzitimiza, kutoa sadaka na zaka na kutubu. Kumwelekea jirani kwanza ni matendo saba ya huruma ya kimwili, ndiyo, kuwalisha wenye njaa, kuwapa cha kunywa wenye kiu, kuwakaribisha wageni, kuwapa cha kuvaa walo uchi, kuwatazama wagonjwa, kuwatazama wafungwa na kuwazika wafu. Kishapo kuna matendo saba ya huruma ya kiroho: kuwafundisha wajinga, kuwashauri wenye mashaka, kuwaonya wakosefu, kuvumilia magumu, kuwavumilia wasumbufu, kuwafariji wenye dhiki na kuwaombea wazima na wafu. Haya ndiyo ndiyo matendo halisi na si maneno au busu tu.
Kuyafanikisha matendo haya, kunahitaji imani na dhati na katika kuyatenda wakati mwingine kuna kuambatana na maumivu au mateso. Ndiyo kisa tunasoma walipokuwa wakikutana na Wakristo, hawakuwa wanasahau kufanya imara roho zao na kuwaonya wakae katika imani, na kuwatanabaisha wazi wazi ilivyowapasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Ila tufahamu kuwa Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nasi. Na katika ulimwengu mpya, atafuta kila chozi katika macho ya wamchao. Mauti hayatakuwapo tena; wala maombolezo wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yatakuwa yamekwisha kupita.
SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristo, tunakushukuru kwa kutupatia amri ya mpya ya mapendo ambayo tukimakinika nayo tutafaulu kufika katika maskani yako mbinguni. Basi, utufundishe kuiishi kwa vitendo na si porojo na kujisifu kwa maneno tu. Amina.
0 Comments