Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima ya huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, “Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu.” Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi; wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:23-24, 26-27, 29-30
- Wakuu nao waliketi wakaninenea,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako,
Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
K: Heri walio kamili njia zao.
- Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundishe amri zako.
Unifahamishe njia ya mahusia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako. (K) - Uniondolee njia ya uongo ,
Unineemeshe kwa sheria yako.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. (K)
INJILI: Yn. 6:22-29
Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja; tena ya kuwaYesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao. Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru. Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, “Rabi, wewe umekuja lini hapa?”
Yesu akawajibu, akasema, “Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu.” Basi wakamwambia, “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?” Yesu akajibu, akawaambia, “Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.”
TAFAKARI
FANYIENI KAZI CHAKULA KINACHODUMU : Kumbukumbu ya Mtakatifu Atanasi, mshiriki wa mtaguso wa Necea na mtetezi wa imani katika umoja na usawa kati ya Mungu Mwana na Mungu Baba, inatupa taswira sawa na somo la kwanza. Mtakatifu Stefano, kwa kuongozwa na nguvu na busara ya Roho wa Mungu, anatenda ishara kubwa. Wapinzani wake wanajaribu kushindana naye, na Stefano anadhihirika kuwa mwenye hekima na utukufu, na wanashindwa. Katika Injili, Yesu anawaambia wanaomtafuta kwamba wasikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali kidumucho hata uzima wa milele.
Tukio hili la Mtakatifu Stefano ni mfano halisi, kati ya kundi linalofuata mafundisho ya kibinadamu na kutafuta mambo yanayopita. Kwenye upande mwingine kuna Mtakatifu Stefano na Yesu Kristo, wanaotendea kazi mambo yanayodumu milele. Tunaalikwa kutumia muda wetu mwingi kutendea kazi mambo yanayodumu hadi ufalme wa milele.
SALA: Ee Mungu, utujalie kutafuta daima chakula kunachodumu hadi ufalme wa milele
0 Comments