Siku zile, mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, “Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.” Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, “Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, ‘Ondoka; Petro, ukachinje ule.’ Nikasema, ‘Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu.’ Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, ‘Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.’ Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, ‘Yohane alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatiza kwa Roho Mtakatifu.’ Basi, ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, ‘Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.’”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 42:1-2, 43:2-3
- Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji,
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
- Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K) - Nilitewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako. (K) - Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
Nitakusifu kwa kinubi, ee Mungu, Mungu wangu. (K)
INJILI: Yn.10: 11-18
Yesu alisema: “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwamwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.”
TAFAKARI
UKOMBOZI WA KRISTO HAUNA MATABAKA :
Mtume Paulo anaeleza kwa nini aliwatembelea mataifa. Aliongozwa na Roho wa Mungu, kwa ushuhuda malaika. Katika injili, Yesu akijielezea kuwa Mchungaji Mwema anayetoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Aanasisitiza, “Na kondoo ambao sio wa zizi hili, nao pia imenipasa kuwaleta.” Upendo wa Mungu kupitia kwa Yesu Kristo Mfufuka hauna mipaka. Wote watakuwa kundi moja na mchungaji mmoja. Mapendo ya Mungu ni makuu kwa kila mmoja anayesikia sauti yake na kujiunga na familia ya Baba Mmoja, na hakuna asiyestahili ukombozi.
Wote walioisikia sauti ya Mchungaji Mwema wanakubalika katika kundi lake. Kristu Mfufuka, kwa upendo wake mkuu, kupitia uchungaji wa Kanisa lake, anawakumbatia na kuwapokea wote wanaokuja kwake. Kutokaa na haya tunaombwa tumkubali Kristo kwa kuwa atatukomboa na kutuweka huru.
SALA: Ee Mchungaji Mwema, uwajalie waumini wako kuisikia sauti yako. Uwajalie upendo usiokuwa na mipaka, ili wote wawe chini yako, kama kundi moja.
0 Comments