Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha. Akaniambia; “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.” Lakini nikasema, “Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu.” Na sasa Bwana asema hivi, “Yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena”; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, “Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 139:1-3, 13-15
- Ee Bwana umenichunguza na kunijua
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepete kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K)Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.
- Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu. (K) - Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu haikusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri,
Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi. (K)
SOMO 2: Mdo. 13 : 22-26
Paulo alisema, “Mungu alimwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia,” akisema, “nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake.” Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, “Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.” Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.
INJILI: Lk. 1:57-66, 80
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema, “La, sivyo; bali, ataitwa Yohane.” Wakamwambia, “Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo.” Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohane. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.” Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.
TAFAKARI
NGUVU, UJASIRI, UKWELI NA UTUME WA INJILI: ‘Bwana ameniita tangu tumboni mwa mama yangu.’ Yohane Mbatizaji ni mfano halisi ya nabii aliyeandaliwa tangu tumboni. Alisifika kwa umahiri katika utume wake. Alitungwa na kuzaliwa kimuujiza kwa wazee Zakaria na Elisabeti. Alimtanguliza Kristo katika kuzaliwa, kuhubiri toba, na ufiadini. Aliruka tumboni tangu mamake Elizabeti anapoisikia sauti ya Bikiria Maria. Alifunga Agano la kale na kufungua agano jipya. Alimwandalia Kristo njia kwa kuwabatiza waliotubu na kumtambulisha kwa watu alipotokea. Alisubiri kwa hamu ujio wa Kristo. Alimbatiza na kwa msaada wa sauti ya Mungu akamtambulisha kama ‘Mwanakondoo wa Mungu’ na kujishusha. Aliishi maisha ya umaskini kwa chakula na mavazi duni, lakini alijawa na neema za Mungu ndani mwake. Aliendelea kusimamia ukweli hadi kifodini chake.
Tunahimizwa kwa maisha yake kujituma kwa nguvu, ujasiri na haki kutenda tunaloliamini.
SALA: Ee Bwana utujalie kuujua, kuuthamini na kuuishi wito wetu.
0 Comments