Ad Code

Masomo ya misa Septemba 21,2022; Jumatano: Juma La 25 La Mwaka

SOMO 1: Efe. 4:1-7, 11-13

Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wenu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 19:2-3, 4-5

  1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
    Na anga laitangaza kazi ya mikono yako.
    Mchana husemezana na mchana,
    Usiku hutolea usiku maarifa.

K: Sauti yao imeenea duniani mwote.

  1. Hakuna lugha wala maneno,
    Sauti yao haisikilikani.
    Sauti yao imeenea duniani mwote,
    Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)

INJILI: Mt. 9:9-13

Yesu alipokuwa akipita aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, “Nifuate.” Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Naye aliposikia, aliwaambia, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya: Nataka rehema, wala si sadaka. Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

TAFAKARI
MWALIKO WA KUMFUATA YESU: Leo tunaadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Mathayo mtume. Katika Injili, huyu mtoza ushuru aliyehesabika kama mdhambi katika jamii ya Mafarisayo, anaitwa na Yesu. Jina Mathayo lina maana ya zawadi ya Mungu. Badala ya jamii kumwona kama mdhambi tu walipaswa kumpokea kama zawadi ya Mungu kwa jamii yao, kwa sababu uwepo wake unakuwa ishara ya wokovu wa jamii yote. Mathayo anapoitwa anaacha kila kitu na anamfuata Yesu bila kutoa kisingizio chochote. Matayo anatufundisha kuwa kumfuata Yesu kunahitaji moyo wa sadaka na kujitenga na mambo mengine mengi ya kidunia. Matayo aliacha ofisi yake ya ushuru, akamfuata Kristo. Kwa ubatizo wetu tuliitwa kumfuata Yesu na kuyaacha yote mengine. Tunapokiri Kanuni ya Imani tunakubali kuacha yote yasiyoendana na Kristo na hivyo kujitoa kikamilifu kwa ajili ya Kristo. Tusirudi nyuma.

SALA: Bwana Yesu, niongoze nikufuate kwa uaminifu mpaka mwisho. Amina.

Post a Comment

0 Comments