Ad Code

Masomo ya Misa Septemba 30,2022; Ijumaa: Juma La 26 La Mwaka

Mt. Hieronimo, Padre na Mwalimu wa Kanisa


SOMO 1: Ayu. 38:1, 12-21, 40:3-5

Ndipo Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, waovu wakung’utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, vitu vyote vinatokea kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Je! Umefunuliwa malango ya mauti, au umeyaona malango ya kuzimu? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote. Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi? Upate kuipeleka hata mpaka wake, upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, na hesabu ya siku zako ni kubwa!” Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, “Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu; naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 139:1-3,7-10,13-14

  1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
    Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
    Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
    Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
    Umeelewa na njia zangu zote.

K: Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.

  1. Niende wapi nijiepushe na roho yako?
    Niende wapi niukimbie uso wako?
    Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
    Ningefanya kuzimu kitanda change, Wewe uko. (K)
  2. Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
    Na kukaa pande za mwisho za bahari;
    Huko nako mkono wako utaniongoza,
    Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)
  3. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
    Uliniumba tumboni mwa mama yangu.
    Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
    Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. (K)

INJILI: Lk. 10: 13-16

Yesu aliwaambia wafuasi wake:
 “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

TAFAKARI
UMUHIMU WA KUPOKEA NENO LA MUNGU: Katika utume alioufanya Yesu hapa duniani, alizunguka maeneo mbalimbali akifundisha watu na kuwatakia wongofu. Alitenda miujiza mingi ili kuwaimarisha. Kwa bahati mbaya Yesu alishuhudia baadhi ya watu katika miji kushupaa katika uovu wao na kukataa kufanya toba na hivyo kukataa wongofu. Walijikita katika tamaduni zao na mila zao wakakataa mwaliko wa Yesu kubadili namna waishivyo. Yesu anailinganisha miji hii ya Korazini na Bethsaida na Tiro na Sidoni kwani ililaaniwa na Manabii kwa kutowapokea wajumbe wa Mungu (Isa 23:1, Yer. 25:22, Amo 1:10). Ole hii anayoitangaza Yesu inatualika tufanye mabadiliko ya tunavyoishi, tukubaliane na wajumbe wanaotumwa kwetu kwani wanakuja kwa jina la Yesu. Mapadre wetu wanapotumwa, hutoa huduma kwa niaba ya Kristo. Tukiwapokea vizuri na kuwasikiliza, tunampokea Yesu mwenyewe na tukiwakataa tunamkataa Yesu aliyewatuma. Tusifanye migumu mioyo yetu kwani adhabu ya Mungu itakaa juu yetu.

Post a Comment

0 Comments