Ad Code

MASOMO YA MISA, OKTOBA 20, 2022 ALHAMISI, JUMA LA 29 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Efe.. 3:14 – 21

Nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani.
Kristo akae mioyoni mwenu kwa Imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.
Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu, naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 33:1 – 2, 4 – 5, 11 – 12, 18 – 19 (K) 5

(K) Nchi imejaa fadhili za Bwana.

Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. (K)

Kwa kauwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)

Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake. (K)

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

SHANGILIO
Yn. 17: 17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.

INJILI
Lk. 12:49-53

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!
Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katiak nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, nab inti na mamaye; mkwe na mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

0 Comments