Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano ya rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki i na wewe lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 79:8-9, 11, 13
- Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumeadhilika sana.
(K)Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana. - Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K) - Kuugua kwake aliyefungwa na kuingie mbele zako.
Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)
INJILI: Lk 6:36-38
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.
TAFAKARI:
KUWA NA HURUMA: Huruma ni wema ulio tayari kusaidia na kusamehe. Mungu ni wa huruma, na tena ndiye huruma yenyewe. Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma (Lk 6:36). Kipndi hiki cha kwaresima tunaalikwa tuwasaidie wahitaji wa aina zote kwa ajili ya Kristo na kama vile tunamhudumia Kristo mwenyewe. Tunapowasaidia watu kwa upendo tutajikuta pia hata kusamehe ni rahisi. Tunapoambiwa kuwa na huruma kwa wenzetu, maana yake ni kumuiga Mwenyezi Mungu aliye mwingi wa huruma kwetu sisi wanadamu. Mungu yupo tayari kutusaidia na kutusamehe wakati wote. Tunapotafakari huruma ya Mungu kwetu katika maisha yetu kama watenda dhambi, hatuna budi nasi kuwaonea wenzetu huruma. Yesu anatukumbusha ya kwamba, uhusiano wetu na Mungu, ni lazima uhusishwe na uhusiano wetu na ndugu zetu katika maisha yetu ya kila siku. Inafaa tuhurumiane, tupendane, na tujali hali za wenzetu. Kama haingekuwa huruma ya Mungu sisi hatungehurumiana. Na kama hatungehurumiana, bila shaka tungetendeana maovu hata mauaji. Kwenye dunia ya aina hiyo, tungekuwa wapi sisi wanadamu wanyonge?
SALA: Kwa neema yako ee Bwana, tuwezeshe kuwa na huruma kwa ndugu zetu.
0 Comments