SOMO 1
Mdo. 2:14, 22 – 28
Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.
Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkasulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake.
Nalimwona Bwana mbele yangu sikuzote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.
Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 16:1 – 2, 5, 7 – 11 (K) 11
(K) Utanijulisha njia ya uzima.
Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu. (K)
Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)
Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutaiachaia kuzimu nafsi yangu.
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele. (K)
SOMO 2
1Pet. 1:17 – 21
Ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwanakondoo asiye na ila, asiye na waa, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata Imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 24:32
Aleluya, aleluya,
Bwana Yesu, utufunulie maandiko; uwashe mioyo yetu unaposema nasi. Aleluya.
INJILI
Lk. 24:13 – 35
Siku ile watu wawili miongoni mwa wafuasi wa Yesu walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.
Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.
Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.
Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?
Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni, nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 Comments