Ad Code

MASOMO YA MISA APRILI 4, 2023; JUMANNE: JUMA KUU mazengo / 56

SOMO 1: Isa. 49:1-6

Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; Akaniambia; wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena. Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 71:1-6, 15, 17

  1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
    Nisiaibike milele.
    Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
    Unitegee sikio lako, uniokoe.
    (K) Kinywa changu kitasimulia wokovu wako.
  2. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
    Nitakakokwenda siku zote.
    Umeamuru niokolewe,
    Ndiwe genge langu na ngome yangu.
    Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
    Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)
  3. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
    Tumaini langu tokea ujana wangu.
    Nimekutegemea wewe tangu kuzaliwa,
    Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
    Ninakusifu Wewe daima. (K)
  4. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
    Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
    Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
    Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)

INJILI: Yn. 13:21-33, 36-38
Pale alipokuwa na mitume wake mezani Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti. Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye. Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua tunavyohitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu. Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku. Basi huyo alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara. Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi ya kwamba, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja; kadhalika sasa nawaambia ninyi. Simoni Petro akamwambia, Bwana, unakwendapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye. Petro akamwambia, Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako. Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.

TAFAKARI:
HUWA NI USIKU TUNAPOMWACHA BWANA: Mazungumzo ya Yesu na Mitume wakati wa Karamu ya Mwisho, yanazua maswali mengi kwenye akili ya mitume na mashaka pia. Jambo la kumsaliti mwalimu na Bwana wao halikuwa jambo dogo. Ndio maana Simon Petro hajatulia kabisa baada ya kusikia kauli ya Kristo ya kuwa mmoja wa Mitume atamsaliti. Anamwagiza mtumwa ambaye Yesu alimpenda, kudadisi zaidi na kujua ni nani hasa. Petro tayari ameanza kazi ya kuliongoza Kanisa. Yuda Iskariote anaanza kuitekeleza kazi yake ya kumsaliti Yesu pale anapopata tonge. Bwana anaelewa kabisa sadaka anayotoa kwani ndiye ajitoaye kwa hiari yake. Mwinjili Yohane anaeleza kuwa mambo haya yalifanyika usiku. Kumbe mara nyingi huwa ni nyakati za usiku katika maisha yetu ya kiimani ndipo sisi humwacha Mungu na kuingia na yule mwovu? Kwa unyenyekevu, tuukubali upendo wa Mungu kwetu uliomfanya amtoe Mwanawe wa Pekee atukomboe. Tusimwache bwana kamwe kiroho kwani tukifanya hivyo tutapatana na shetani na kuanguka kwenye majaribu.

SALA: Ee Bwana, tujalie kukufuata daima pasi na kukuondokea, ili tuweze kuurithi Uzima wa Milele.

Post a Comment

0 Comments