KUTABARUKIWA BASILIKA LA LATERANI
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Eze 43:1-2, 4-7
Malaika alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 122: 1-5, 7-8
Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)
Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)
Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
Niseme sasa, Amani ikae nawe.
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu,
Nikutafutie mema. (K)
SOMO 2: 1 Kor 3:9-13, 16-17
Ninyi ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
INJILI: Yn 2:13-22
Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu alikwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuoneshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.
TAFAKARI:
KANISA LINAPASWA KUHESHIMIWA: Leo Kanisa linakumbuka kwa heshima kutabarukiwa Basilika la Laterani. Huenda baadhi yetu tumeshashuhudia jinsi makanisa yanavyobarikiwa na mengine, Altare kuwekwa wakfu. Hili huwa ni tukio zito na linalofanyika kiibada. Yote haya ni kuonyesha umuhimu na uzito wa sehemu yenyewe kuwa ni tofauti kabisa na majengo mengine kama kumbi za sherehe au mikutano na hivi kututaka tupaheshimu daima. Ndio maana Yesu alipoona watu wametumia sivyo lile hekalu, tunaelezwa aliwafukuza. Hilo lilimkera na kumghadhibisha. Paulo katika somo la pili ametukumbusha kuwa miili yetu ni hekalu la Mungu, tusiiharibu. Ulimwengu wa leo unawasifu wanaoichezea miili yao, na hata wanataka kuyabadili maumbile, zikiwemo jinsia. Mume anataka ajigeuze awe mke na vivyo hivyo kwa mwanamke. Huko ni kumkebehi Mungu, kumkasirisha na kumfanya atamani kutufukuza na kututoa nje kwa hasira. Tujue miili yetu imebeba sura na mfano wa Mungu.
SALA: Bikira Maria Mama wa Kanisa, tuombee neema ya kuwa na heshima kwa Kanisa na kutunza miili yetu.Amina.
0 Comments