Ad Code

MASOMO YA MISA DESEMBA 5, 2023; JUMANNE: JUMA LA 1 LA MAJILIO


Mt. Saba, Mkaa Pweke Urujuani

Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa. 11:1-10
Siku ile likatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.
Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.
Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzika patakuwa na utukufu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 72: 1-2, 7-8, 12-13

  1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
    Na mwana wa mfalme haki yako
    Atawaamua watu wako kwa haki,
    Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

K: Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
na wingi wa amani kwa milele.

  1. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
    Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
    Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
    Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)
  2. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
    Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
    Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
    Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)
  3. Jina lake na lidumu milele,
    Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
    Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
    Na kumwita heri. (K)

INJILI: Lk. 10:21-24
Siku ile, Yesu alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.
Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.

TAFAKARI:
KILA MTU ANA BAHATI YAKE: Nabii Isaya katika somo la kwanza anazungumzia watu wenye tabia ya kuamua mambo bila haki. Kuna mtu ambaye akisikia jambo bila hata ya kufanya uchunguzi kupata uhakika na kujua hali halisi, unakuta anatoa hukumu. Raisi mstaafu wa Tanzania mheshimiwa Jakaya Kikwete, aliwahi kusema, “Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.” Alimaanisha kuwa usione tu jambo na kutoa hukumu, tenda haki kwa kuliwaza na kuliamulia wewe binafsi. Yesu katika Injili anawadhihirishia wanafunzi wake kuwa, wana bahati ya pekee kwa yale yaliyofuniliwa kwao. Anawasihi wasifanye mzaha na kuyapuuzilia mbali. Hii kwao ni bahati kweli na ndipo anasema, “Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi.” Hii bahati tuliyo nayo kila mmoja wetu, tusiipuuzilie. Tunaalikwa kujitazama na kujiuliza, tuna bahati gani tumejaliwa katika maisha na tumezitumiaje?

SALA: Baba wa Mbinguni, tunaomba utupe macho maangavu ili tutambue na kuthamini yale unayotujalia katika maisha yetu. Amina.

Post a Comment

0 Comments