Kwanza kabisa nianze kwa kusema kuwa, tangu kale Wachungaji wa zamani walikuwa wanatumia fimbo kwa ajili ya kuchungia mifugo pindi wawapo malishoni. Fimbo hiyo ilikuwa na kazi kubwa sana hasa zaidi ilitumika kuwaongoza wanyama njia sahihi ya kupita, na wakati mwingine hugeuka na kuwa silaha pale wanyama wa mwituni wanaposhambulia kundi.
Hivyo hata Kanisa nalo linaamini kwamba, Askofu ndiye Mchungaji mkuu wa Kanisa na jukumu lake haswa ni kuchunga kondoo (Waamini) wasipotea, na kulilinda Kanisa lisianguke kutokana na mafundisho ya uongo yanayotolewa kila siku dhidi yake. Na ndio maana Askofu anapewa fimbo kama ishara kamili ya kulisimamia Kanisa na kulitetea pale hatari ya kiimani inapojitokeza.
𝗦𝘄𝗮𝗹𝗶: 𝗦𝗮𝘀𝗮 𝘂𝘁𝗼𝗳𝗮𝘂𝘁𝗶 𝗸𝗮𝘁𝗶 𝘆𝗮 𝗳𝗶𝗺𝗯𝗼 𝘆𝗮 𝗔𝘀𝗸𝗼𝗳𝘂 𝗻𝗮 𝗶𝗹𝗲 𝘆𝗮 𝗣𝗮𝗽𝗮 𝗻𝗶 𝗶𝗽𝗶?
𝗝𝗶𝗯𝘂: 👇👇👇👇👇👇👇
Mpendwa, fimbo ya Askofu mara nyingi huitwa "CROSIED" ambalo limetokana na neno la Kilatini "CROCIA" lenye maana ya "MKUNJO" kwa Kiswahili. Hivyo fimbo zote za Maaskofu ukiziangalia vizuri, utazigundua kuwa zina mikunjo juu yake na zingine katikati ya hiyo mikonjo zinakuwa na Misalaba ila sio zote.
Daima fimbo hii anayoitumia Askofu huonesha mamlaka ya kiuchungaji aliyekuwa nayo Askofu katika Kanisa. Pia fimbo hizi huwezi kuzikuta hovyo hovyo, hadi pale panapokuwa na maadhimisho ya Misa ya Kiaskofu.
Kadhalika fimbo ya Papa nayo huitwa fimbo ya kiuchungaji, na ina maana sawa na ile ya Askofu. Kwani kimsingi Papa naye ni Askofu kama ilivyo kwa Maaskofu wengine, licha ya kupewa jukumu la kuliongoza Kanisa katika cheo hicho cha Upapa.
Ukweli ni kwamba, fimbo ya Papa hapo zamani ilifanana mno kama ile anayoitumia Askofu na kuzitofautisha ilikuwa ngumu sana. Lakini mwaka 1978 wakati wa Papa Paulo VI, fimbo ya Papa ilibadilishwa kidogo ili kuitofautisha na ile ya Askofu, ambayo yenyewe daima huwa na Msalaba juu yake pasipokuwa na mikunjo yoyote. Utaratibu ambao unatumika hadi hivi leo.
𝗧𝗨𝗠𝗦𝗜𝗙𝗨 𝗬𝗘𝗦𝗨 𝗞𝗥𝗜𝗦𝗧𝗢...
0 Comments