Ad Code

MASOMO YA MISA, APRIL 27, 2022

DOMINIKA YA 8 YA MWAKA C WA KANISA


MWANZO:

Zab. 18:18-19


Bwana alikuwa tegemeo langu, akanitoa akanipeleka panapo nafasi, akaniponya kwa kuwa alipendezwa nami.


SOMO 1

YbS. 27:4-7


Kutikisa chekecheke, itabaki wishwa; vile vile ila za mtu katika kujadili. Tanuu hujaribu vyombo vya mfinyanzi; Vile vile jaribio la mtu ni kujadili. Matunda ya mti huonyesha ulimaji wake; Vile vile kujadili mawazo ya moyoni. Usimsifu mtu usijemsikia anajadili; Hakika hilo ni jaribio la wanadamu.


Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI

Zab. 91:1 – 2, 12 – 15 (K) 1


(K) Ni neno jema kumshukuru Bwana.


Ni neno jema kumshukuru Bwana,

Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.

Kuzitangaza rehema zako asubuhi,

Na uaminifu wako wakati wa usiku. (K)


Mwenye haki atasitawi kama mtende,

Atakuwa kama mwerezi wa Lebanoni. (K)


Waliopandwa katika nyumba ya Bwana

Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.

Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,

Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.

Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili,

Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu. (K)


SOMO 2

1Kor. 15:54 – 58


Wapenzi, uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa, lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? Uwapi, Ewe mauti, uchungu wako? Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakni Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.


Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO

Mt. 4:23


Aleluya, aleluya,

Kristu alihubiri habari njema ya ufalme na kuponya wagonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.

Aleluya.


INJILI

Lk. 6:39-45


Yesu aliwaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.


Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

0 Comments