Mpendwa! Kwa kawaida Majilio ni kipindi cha matayarisho kwa ajili ya kuzaliwa Masiha. Lakini hata hivyo Kanisa halitafakari tu kuzaliwa kwake na kuishia hapo, bali linawatayarisha Waamini wajiandae kwa ajili ya Ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Hivyo katika kipindi hiki cha Majilio, Mama Kanisa anatumia mafundisho ya Nabii Isaya ili kutuhimiza tumtumaini Mungu ipasavyo na kuachana na mambo ya kipagani, mwenendo mbaya na hivi kumfuasa Kristo katika maisha ya Utakatifu.
Daima mafundisho hayo yanatualika tuongoke, na kuwa tayari muda wote kumsubiri Masiha. Kama vile Nabii Isaya alivyowatayarisha watu wa enzi yake kumtumainia Mungu, basi ndivyo leo hii Mama Kanisa anavyotuandaa vema ili tumpokee Bwana Yesu ndani ya mioyo yetu isiyo na mawaa.
Kwahiyo kielelezo hicho cha matayarisho ya Noeli (yaani Ujio wa Yesu),kuna desturi ya kuwasha mishumaa minne ndani ya Kanisa Katoliki, kipindi chote cha Majilio.
Kwa ujumla mishumaa ni uwepo wa Mungu katikati ya mataifa na ndani yetu pia, na ndiyo maana tunasema Mungu ni wa milele, kama ilivyo ile Taa ya milele iwakayo pembezoni mwa Tabernakulo, inavyoashiria uwepo wa Kristo katikati yetu.
Basi kipindi hiki cha Majilio tunawasha mishumaa minne, ili kuwakilisha miaka 1000 ambayo mwanadamu aliweza kuusubiria Ujio wa Yesu Kristo ulioahidiwa na Mungu mwenyewe pale bustanini Edeni mpaka Unabii huo ulivyoweza kutimia. (Rejea Mwanzo 3:15).
Pia tunaambiwa kwamba katika safari hii ya Majilio, wapo watu muhimu wanaotuongoza na ambao tunapaswa kuwafuata kila siku ili tukutane na Kristo.
Hivyo basi pamoja na mambo hayo mengi ya Kilitrujia, tabia hii ya kuwasha mishumaa ndani ya kipindi hiki, ni namna pia ya kutambua na kuenzi nafasi za watu hao katika kuwatayarisha Wanadamu kwa Ujio wa Kristo.
Na ndiyo maana mishumaa hiyo minne inawashwa, ili kutukumbusha yale yaliyofanywa na kutangazwa na watu hao, katika kutukutanisha na Mwokozi wetu.
1. MSHUMAA WA KWANZA, HUITWA MSHUMAA WA NABII ISAYA.
Mpendwa! Isaya daima ni Nabii wa matumaini, mwenye kipaji cha kutokeza matazamio ya mwanadamu na kumhakikishia atatimizwa na Mwokozi.
2. MSHUMAA WA PILI, HUITWA MSHUMAA WA YOHANE MBATIZAJI.
Huyu ndiye Nabii aliyemtangulia Masiha ili kuandaa njia yake. Yeye ni mwenye kuhimiza toba, kwa kuwa tunapaswa kupindua maisha yetu ili tukutane vema na Kristo.
Wote twatambua kuwa, nafasi ya Yohane Mbatizaji katika kuandaa Ujio wa Yesu Kristo, daima alikuwa ni mtangulizi mnyenyekevu, anayetualika leo hii tutengeneze njia zetu kwa ajili ya Ujiowa pili wa Bwana Yesu.
Hivyo Yohane Mbatizaji aliweza kumtambulisha Masiha kwa watu, na leo hii kwa namna ya pekee anatutafakarisha na kutuandaa vema kwa mahubiri yake, ili tuweze kuongoka na kumpokea Bwana.
3. MSHUMAA WA TATU, HUITWA MSHUMAA WA MTAKATIFU YOSEFU.
Mpendwa! Hatuwezi kuyazungumzia maisha ya Yesu, bila kumtaja Mtakatifu Yosefu. Maana huyu ndiye Baba mlishi wa Yesu na Mume wa Bikira Maria.
Yosefu alikuwa ni Baba mnyenyekevu asiye na makuu, na kwa namna hiyo katika unyenyekevu wake huo, aliweza kutekeleza Mpango wa Mungu katika kumlinda na kumlea Mtoto Yesu.
Na ndiyo maana Mama Kanisa pia anatualika, tumuone Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa Maisha, kupitia mifano bora ya Mtakatifu Yosefu.
4. MSHUMAA WA NNE, HUITWA MSHUMAA WA BIKIRA MARIA.
Mwisho katika dominika ya nne ya Majilio, mama Kanisa anawasha mshumaa huu ili kutuonyesha kuwa, Bikira Maria alikuwa ni Mama wa Mkombozi asiye na doa (yaani dhambi).
Hivyo Mama huyu anatufundisha kwamba, ili tumfuate Kristo basi ni lazima tujitoe kikamilifu bila kujibakiza, katika kutekeleza Mapenzi ya Mungu maishani mwetu.
Na ndiyo maana Bikira Maria baada ya kutokewa na Malaika Gabriel (Angelus), na kupashwa habari kuwa atakuwa Mama wa Mungu, alisema:
"Mimi ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyonena" (Rejea Luka 1:38).
Kumbe kwa maneno hayo tunaona kuwa, Maria muda wote alikuwa tayari kumpokea Masiha na hata kushiriki naye kwenye Mateso ya Njia ya Msalaba, ili kutimiza Mpango wa Mungu wa kuwakomboa Wanadamu.
Mwisho niseme tu, tunapotafakari kipindi hiki cha Majilio, basi ni vema tufahamu kuwa, hiki ni kipindi kizuri cha kututafakarisha kuhusu Ujio wa pili wa Yesu Kristo.
Kwa sababu hata masomo ya majuma yote manne, yanaendelea kutuasa tujiweke tayari kumpokea Bwana Yesu atakapokuja kwa mara ya pili ulimwenguni.
Mathayo 24:42 inasisitiza kuwa: "Tukeshe na kuomba kila siku, kwa kuwa hatujui siku wala saa atakayokuja Bwana wetu".
0 Comments