Ad Code

Masomo ya misa Juni 22,2022 Jumatano: Juma La 12 La Mwaka

SOMO I: 2 Fal. 22:8-13; 23:1-3

Hilkia, kuhani mkuu, alimwambia Shafani, mwandishi, “Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya Bwana.” Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma. Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, “Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaosimamia nyumba ya Bwana.” Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, “Hilkia kuhani amenipa kitabu.” Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, akasema, “Enendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya Bwana ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.” Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa Bwana, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya Bwana. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:33-37, 40

  1. Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako,
    Nami nitaishika hata mwisho.
    Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
    Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.

(K) Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.

  1. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
    Kwa maana nimependezwa nayo.
    Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako,
    Wala usiielekee tamaa. (K)
  2. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa,
    Unihuishe katika njia yako.
    Tazama, nimeyatamani mausia yako,
    Unihuishe kwa haki yako. (K)

INJILI: Mt. 7:15-20

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.”

TAFAKARI
MTAWATAMBUA KWA MATUNDA YAO : Kwa moyo wa toba, mfalme anawakusanya watu baada ya kupatikana kitabu cha torati kilichofichika miaka mingi. Kinasomwa mbele ya viongozi na watu wote na wanaridhia kukifuata. Katika Injili Kristo anawatahadharisha mitume dhidi ya watu wanaojinadi kuwa mitume, lakini wakiwa na nia tofauti. Anawapa mbinu ya kuwatofautisha wa kweli na waigizaji ; ‘mtawatambua kwa matunda yao.’ Mfalme anaonekana kuwa kweli mtu mwema na anayewajali watu anowahudumia. Anawatakia watu wake mema na anapotambua kwamba wamekosa anawaongoza kutubu.
Nyakati zetu ni wengi wanaoibuka na kujitambulisha kama watu wa Mungu na kuna uwezekano mkubwa wa kuwapoteza waumini wenye imani haba. Tutazame matokeo ya kazi yao na tutatambua ni yupi mwenye nia ya kuwaokoa watu na ni yupi mwenye nia ya kuwapoteza.

SALA: Ee Bwana, wajalie watumishi wako kuwa wachungaji wa kweli, na uwape waumini roho wa kuwapambanua mitume.

Post a Comment

0 Comments