Ad Code

MASOMO YA MISA JUNI 1, 2023; ALHAMISI: JUMA LA 8 LA MWAKA

Mt. Yustino, Shahidi

Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: YbS 42:15-25
Sasa nitayanena matendo ya Bwana, nami nitayadhihirisha mambo yale niliyoyaona, kwa neno la Bwana vimekuwapo viumbe vyake, na kazi impendezayo ni sawasawa na amri yake. Jua litoapo nuru hudhihirika mahali pote; na kazi ya Bwana imejaa utukufu wake. Watakatifu wa Mungu hawawezi kuyatangaza maajabu na miujiza yake, walakini Mungu amewapa majeshi yake uwezo wa kusimama mbele ya utukufu wake. Yeye huchunguza vilindi, na moyo wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana aliye juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu, hutujulisha yaliyopita, na yatakayokuja, na kuzifunua alama za mambo yaliyofichwa. Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lo lote ambalo limefichwa naye. Matendo makuu ya hekima yake ameyaratibisha, ambaye, Yeye ni mmoja tu, tangu milele na hata milele; hakuzidishiwa kitu, wala kupunguziwa kitu; wala yeye hana haja ye yote ya mshauri. Ee ajabu ya uzuri wa viumbe vyake! mtu angeweza kuliona hilo hata kwa habari ya cheche. Vitu vyote vyaishi na kudumu daima, na kwa kila haja vyote vyamtii. Vyote vinahitilafiana, wala hakufanya cho chote kisicho kamili; hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio; naye ni nani atakayekinai kwa kuutazama utukufu wake?

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 33:2-9

  1. Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
    Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
    Mwimbieni wimbo mpya,
    Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
    (K) Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika.
  2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
    Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
    Huzipenda haki na hukumu,
    Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
  3. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika,
    Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
    Hukusanya maji ya bahari chungu chungu,
    Huviweka vilindi katika ghala. (K)
  4. Nchi yote na imwogope Bwana,
    Wote wakaao duniani na wamche.
    Maana Yeye alisema, ikawa;
    Na Yeye aliamuru, ikasimama. (K)

INJILI: Mk 10:46-52
Walifika Yeriko; Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

TAFAKARI:
MUNGU NDIYE MUWEZA WA YOTE: Watu maarufu katika jamii hupewa sifa nyingi kadiri ya umashuhuri wao. Katika Somo la Kwanza, tumesikia jinsi Mungu alivyo wa ajabu. Anasifika kwa kufanya maajabu, na kazi zake ni za ajabu pia. Hakuna wa kufanana naye. Katika Injili, kipofu Bartimayo, mwana wa Timayo, anapata kuona. Huyu kipofu alikuwa mwombaji, na jamii ilijua kuwa ni mwombaji wa siku zote. Leo anaposikia kuwa Yesu anapita, kwa kuwa alikuwa na imani naye, na kwa vile anajua uweza na umaarufu wa Yesu, anaamua kuomba kitu kikubwa kitakachomletea furaha maishani. Anaomba apate kuona, apate nuru yaani mwanga. Anajipa moyo anamfuata Yesu huku akimwambia, “Nataka kuona”. Uweza wa Mungu ni mkubwa na wa ajabu. Yeye huwaponya watu katika mazingira yoyote yale hata yaliyoshindikana ambayo hatuwezi kama wanadamu. Tumwombe Mungu atusaidie nasi tupone katika upofu wetu hasa tukosapo kuziona shida za wenzetu. Tuepukane na ukaidi wa kutofuata miongozo ya Kanisa.

SALA: Kwa maombezi ya Mt. Augustino wa Kanterbury Askofu, tuombee tupate neema ili tujaliwe kuutambua uweza wa Mungu na kuuishi daima. Amina.

Post a Comment

0 Comments