SIKUKUU YA KUONGOKA KWA MT. PAULO, MTUME
SOMO 1
Mdo 22:3-16
Paulo aliwaambia makutano, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani wanaume na wanawake. Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami, waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.
Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, akanijia, akasimama karibu nami akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Bwana.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117:1-2 (K) Mk. 16:15
(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aleluya!
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
enyi watu wote, mhimidini. (K)
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 15:16
Aleluya, aleluya,
Niliwachagua ninyi, nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya.
INJILI
Mk. 16:15-18
Yesu alionekana na wale kumi na mmoja, akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Maana ishara hizi zintafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Neno la Bwana… Sifa kwako ee Kristo.
0 Comments